Wednesday, July 4, 2012

TANZANIA SOCIAL NEWS: HALI YA DK. ULIMBOKA YAANZA KUREJEA

AFYA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka imeendelea kuimarika baada ya kupata matibabu nchini Afrika  Kusini na sasa figo zake zimeanza kufanya kazi.Dk Ulimboka alipelekwa nchini huko mwishoni mwa wiki baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kiasi cha kusababisha figo zake kushindwa kufanya kazi.

Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema Dar es Salaam jana kwamba, hali ya Dk Ulimboka imeimarika na kuwaomba Watanzania wamuombee apone haraka.“Taarifa tulizozipata kutoka Afrika Kusini zinasema kwamba,  hali ya Dk Ulimboka imezidi kuimarika tofauti na alivyokwenda, figo zimeanza kufanya kazi ingawa kwa polepole na amefanyiwa vipimo vingine,” alisema Dk Kabangila na kuongeza:

Awali, chanzo kimoja cha habari kilidokeza kwamba  hali ya Dk Ulimboka imeimarika kutokana na kupatiwa huduma za matibabu kwa haraka kwa kufanyiwa pamoja na vipimo vingine, kile cha usafishaji damu na figo (Dalysis), mara kwa mara. Kabla ya kuondoka nchini, Dk Ulimboka alifanyiwa usafishaji huo mara mbili.

Madaktari walisema kuwa, kipimo hicho kililenga  kupunguza kiwango cha sumu iliyoonekana  kwenye damu, ambayo haikutambulika mara moja kama ilitengenezwa ndani ya mwili au vinginevyo kwa kuwa hakuna kipimo cha kubaini tatizo hilo nchini.

CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI

TANZANIA POLITICAL NEWS: DRC INATAKIWA KUSHUGHULIKIA IPASAVYO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inatia wasiwasi na hivyo Tanzania inafuatilia kwa makini hali inavyoendelea katika eneo hilo la nchi hiyo jirani.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania ingependa kuona hali ya amani inarejea katika DRC kwa sababu nchi hiyo inahitaji kupata muda wa amani ili waelekeze nguvu zake kwenye maendeleo badala ya kupigana.

Rais Kikwete amesema hayo jana, Jumanne, Juni 3, 2012, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Profesa Ntumra Luaba Alphonce, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu wa International Conference on Great Lakes Region (ICGLR) kwenye Hoteli ya Roca Golf mjini Bujumbura, Burundi.

Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete alikuwa mjini Bujumbura kushiriki katika Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi na kurejea nyumbani jana, 3 Juni, 2012. Kabla ya kuja hapa, Rais Kikwete alikuwa mjini Kigali, Rwanda, kushiriki katika sherehe za namna hiyo zilizofanyika Julai Mosi, mwaka huu. Rwanda na Burundi zilipata uhuru kutoka kwa Wabelgiji Julai Mosi na Julai 2, mwaka 1962.

Rais Kikwete amemwambia Katibu Mtendaji huyo: “ Kwa hakika hali mashariki mwa Congo inatutia wasiwasi mkubwa na Tanzania inafuatilia kwa makini hali hiyo. Congo imekuwa katika vita muda mrefu kupita kiasi kwa sababu tokea mwaka 1997 imekuwa katika vita mfululizo.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Wakati umefika kwa Congo kutulia ili nguvu inayoingia katika mapambano na vita ielekezwe katika maendeleo ya wananchi wa nchi hiyo.”

Rais Kikwete pia ameunga mkono wazo la kuitishwa kwa mkutano wa mawaziri wa nchi wanachama wa ICGLR ili kujadili hali ilivyo katika mashariki mwa Congo kufuatia ombi la DRC kutaka kuitishwa kwa mkutano huo.

Hali katika mashariki mwa Congo imeanza kutia wasiwasi baada ya kikundi cha waasi wa Serikali ya nchi hiyo wakiongozwa na jambazi la kivita John Bosco Ntaganda kuanza tena harakati zake za kivita dhidi ya Serikali ya Rais Joseph Kabila.

Usiku wa jana, Jumanne, Julai 3, 2012, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa DRC,Mheshimiwa Kabila kuhusu hali ilivyo mashariki mwa DRC. Wakati akiwa Kigali, Rwanda,mwishoni mwa wiki, Rais Kikwete pia alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Paul Kagame kuhusu hali ilivyo mashariki mwa DRC.

Aidha, usiku huo huo wa kuamkia jana, Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Mheshimiwa Didier Reynders ambaye pia anahusika na masuala ya nchi za nje, biashara ya nje na masuala ya Umoja wa Ulaya (EU).

Katika mazungumzo Rais Kikwete na Mheshimiwa Reynders walizungumzia hali ya mashariki mwa Congo pamoja na mchakato wa ushirikiano ndani ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu.
Dar es Salaam.
4 Julai, 2012

TANZANIA SOCIAL NEWS: UNESCO YAKUBALI OMBO LA TANZANIA KUHUSU SELOUS GAME RESERVES

Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO katika kikao chake cha 36 kinachoendelea (tarehe 24 June hadi 6 Julai 2012) katika jiji la Saint Petersburg nchini Russia imelikubali ombi la Tanzania la kuurekebisha mpaka wa Pori la Akiba la Selous, ambalo ni Eneo la Urithi wa Dunia, ili kuruhusu uchimbaji wa Madini ya Urani. 

Eneo linalohusika ni asilimia 0.8 ya eneo la Pori la Akiba la Selous

Kwa mara ya kwanza ombi hilo lilipelekwa kwa Kamati hiyo ya Urithi wa Dunia ya UNESCO mwezi Januari 2011 ambapo lilijadiliwa katika Kikao chake cha 35 ambacho kilihamishia mjadala huo katika Kikao cha 36 kinachoendelea.

Uamuzi huo ulifanyika ili kuruhusu Tathmini ya Athari ya Mazingira (EIA) kukamilishwa na kutoa muda kwa wataalam wa IUCN kufika eneo linalihusika ili kuliona na kuhakiki taarifa ya tathmini hiyo.

Pori la Akiba la Selous ambalo lina ukubwa wa Kilomita za Mraba 50,000 ni mojawapo ya hifadhi kubwa duniani zenye viumbe mbalimbali. Ni eneo maarufu kwa nyanda kubwa za tambarare zenye nyasi na misitu ya miombo pamoja na aina nyingi za wanyamapori.

Kufuatia kukubaliwa kwa ombi hilo la nchi yetu nachukua fursa hii kutoa shukrani kwa Kamati ya Urithi wa Dunia, IUCN, Kituo cha Urithi wa Dunia na taasisi mbalimbali, pamoja na watu binafsi ambao walichangia katika kulifanya ombi letu kukubaliwa.

Uamuzi uliotolewa na Kamati ya Urithi wa Dunia utatupatia uwezo na fursa nzuri ya kutimiza malengo yetu kiuchumi na kijamii kwa wananchi. Pia tutapata uwezo wa kulihifadhi na kuliendeleza vyema zaidi Pori la Akiba la Selous.

Mhe Khamis Suedi Kagasheki
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
4 Julai 2012