Temeke imefainikiwa kuilaza Dodoma mabao 2-0 katika mechi ya kundi C ya michuano ya Copa Coca-Cola iliyochezwa leo (Julai 3 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Mabao ya washindi ambao kwa matokeo hayo sasa wamefikisha pointi tano yalifungwa dakika ya tano Hassan Kabunda wakati la pili lilifungwa dakika ya 34 na Abdul Hassan.
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam umeshuhudia Morogoro ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Iringa lililofungwa dakika ya 37 na Mutalemwa Katunzi.
Nayo Kilimanjaro imeibuka na ushindi wa bao 1- dhidi ya Tabora katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani. Bao hilo katika mechi hiyo ya kundi D lilifungwa dakika ya 14 na Eric Christopher.
Kwa matokeo hayo Tabora imebaki na pointi tatu baada ya kushinda mechi moja tu dhidi ya Pwani, na imebakiza mechi moja dhidi ya Kusini Unguja ambayo hata ikishinda haiwezi kuingia hatua ya 16 bora.
Nao mabingwa watetezi Kigoma wamejiweka katika nafasi nzuri ya kucheza 16 bora baada ya kuitandika Kusini Pemba mabao 3-1 katika mchezo wa kundi A uliochezwa Uwanja wa Tamco ulioko mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment