Wednesday, July 4, 2012

TANZANIA FOOTBALL NEWS: MJINI MAGHARIBI YATINGA 16 BORA COPA COCA-COLA

Mjini Magharibi imetinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Copa Coca-Cola baada ya leo (Julai 4 mwaka huu) kuilaza Tanga bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
 
Bao la washindi katika mechi hiyo ya kundi B lilifungwa dakika ya 68 na Juma Ally. Kwa matokeo hayo Mjini Magharibi ambayo imemalizika mechi zake imefikisha pointi 13 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine katika kundi hilo.
 
Mbeya imejipatia ushindi wa pili mfululizo katika kundi lake la C baada ya leo kuifunga Mara bao 1-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam. Mshambuliaji John Jerome alifunga bao hilo pekee dakika ya 43.
 
Licha ya ushindi huo Mbeya wameshindwa kukata tiketi ya 16 bora kwani wamemaliza mechi zao wakiwa na pointi sita tu. Timu za Dodoma yenye pointi 12 na Kinondoni ambayo imefikisha pointi 10 na mechi moja mkononi ndizo zilizofuzu kucheza 16 bora kutoka kundi hilo.
 
Pwani imepata ushindi wake wa kwanza katika kundi lake la D baada ya leo kuichapa Kagera mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani. Mabao ya washindi yalifungwa na Cotiveno Ngaga dakika ya 19, Abdallah Juma dakika ya 30 na Salum Ame dakika ya 68.
 
Kagera ambayo imebakiza mechi moja dhidi ya Shinyanga ikiwa na pointi sita ilipata bao dakika ya 42 kupitia kwa Athuman Kassim. Nazo Ruvuma na Arusha zimetoka suluhu katika mechi ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Tamco

TANZANIA FOOTBALL NEWS: WACHEZAJI 11 WAMALIZA MIKATABA COASTAL UNION

Wachezaji 11 wamemaliza mikataba yao ya kuichezea timu ya Coastal Union ya Tanga inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, na sasa wako huru kujiunga na klabu yoyote.
 
Kwa mujibu wa Coastal Union, wachezaji hao ni Ben Mwalala, Samwel Temu, Francis Busungu, Ahmed Shiboli, Lawrence Mugia, Daudi Chengula, Godfrey Mmasa, Mwinyi Abdulrahman, Sabri Ramadhan China, Soud Abdallah na Ramadhan Wasso.
 
Uhamisho wa wachezaji kwa msimu huu ulianza Juni 15 mwaka huu na utamalizika Julai 30 mwaka huu wakati kipindi cha kuanza wachezaji (kwa wasio wa Ligi Kuu) ni kati ya Juni 15 na 30 mwaka huu.
 
Kwa klabu za Ligi Kuu kutangaza wachezaji watakaositishiwa mikataba yao ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu na usajili wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu.
 

TANZANIA FOOTBALL NEWS: YANGA YAKUTANA NA KIPIGO NA URAFIKI CHA 3-2

YANGA ya Dar es Salaam imechapwa mabao 3-2 na Jamhuri ya Pemba katika mchezo wa Kundi B wa Kombe la Urafiki, kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Yanga ambayo imepeleka wachezaji wake wa kikosi cha vijana visiwani humo, hadi mapumziko, ilikuwa tayari nyuma kwa mabao 2-1.

Lakini kipindi cha pili, Yanga B walikuja juu na kucheza soka ya kuvutia, ingawa waliishia kukosa mabao ya wazi.
Mabao ya Jamhuri yalitiwa kimiani na Ally Salum dakika ya 34, Abdallah Othman dakika ya 45 na Mohamed Omar dakika ya 69, wakati mabao ya Yanga yalifungwa na Hamisi Shaaban dakika ya 17 na Nofteli Mwansasu dakika ya 77.

Katika mchezo wa Kundi hilo uliotangulia, Super Falcon ilitoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Zanzibar All Stars. Mabao ya Falcon yalifungwa na Deo Cassian dakika ya 12 na 25, wakati ya All Stars yalitupiwa nyavuni na Ahmad Malik dakika ya 46 na Twaha Mohamed dakika ya 81.

Katika mechi za ufunguzi jana, Simba SC walianza vyema baada ya kuwafunga wenyeji Mafunzo mabao 2-1, wakati Azam ililazimishwa sare ya 1-1 na U23, Karume Boys.

Abdallah Juma, ambaye amepokewa Simba kama Emmanuel Gabriel mpya, alifunga bao la kwanza dakika ya 27 akiunganisha pasi muruwa ya Patrick Kanu Mbivayanga dakika ya 27.

Mshambuliaji huyo mrefu kutoka Ruvu Shooting ya Pwani, alifunga bao la pili dakika ya 44 kwa kichwa, akiunganisha pasi ya Mbiyavanga tena, kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mafunzo walipata bao lao dakika ya 80, mfungaji Jaku Joma.