YANGA ya Dar es Salaam imechapwa mabao 3-2 na Jamhuri ya Pemba katika mchezo wa Kundi B wa Kombe la Urafiki, kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Yanga ambayo imepeleka wachezaji wake wa kikosi cha vijana visiwani humo, hadi mapumziko, ilikuwa tayari nyuma kwa mabao 2-1.
Lakini kipindi cha pili, Yanga B walikuja juu na kucheza soka ya kuvutia, ingawa waliishia kukosa mabao ya wazi.
Mabao ya Jamhuri yalitiwa kimiani na Ally Salum dakika ya 34, Abdallah Othman dakika ya 45 na Mohamed Omar dakika ya 69, wakati mabao ya Yanga yalifungwa na Hamisi Shaaban dakika ya 17 na Nofteli Mwansasu dakika ya 77.
Katika mchezo wa Kundi hilo uliotangulia, Super Falcon ilitoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Zanzibar All Stars. Mabao ya Falcon yalifungwa na Deo Cassian dakika ya 12 na 25, wakati ya All Stars yalitupiwa nyavuni na Ahmad Malik dakika ya 46 na Twaha Mohamed dakika ya 81.
Katika mechi za ufunguzi jana, Simba SC walianza vyema baada ya kuwafunga wenyeji Mafunzo mabao 2-1, wakati Azam ililazimishwa sare ya 1-1 na U23, Karume Boys.
Abdallah Juma, ambaye amepokewa Simba kama Emmanuel Gabriel mpya, alifunga bao la kwanza dakika ya 27 akiunganisha pasi muruwa ya Patrick Kanu Mbivayanga dakika ya 27.
Mshambuliaji huyo mrefu kutoka Ruvu Shooting ya Pwani, alifunga bao la pili dakika ya 44 kwa kichwa, akiunganisha pasi ya Mbiyavanga tena, kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mafunzo walipata bao lao dakika ya 80, mfungaji Jaku Joma.