Sakata la mgomo wa Madaktari katika hospitali ya Rufaa Mbeya, limeendelea kuingia katika sura mpya baada ya Madaktari 72, waliogoma kutimuliwa na bodi ya hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya.
Hatua ya kutimuliwa kwa madaktari hao imekuja baada ya bodi hiyo kuwaandikia barua ya kuwataka kukaa meza moja na kujadili mstakabali mzima wa madai yao ambapo wadaktari hao kukaidi wito huo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dr. Norman Sigalla, alisema kuwa wameamua kusitisha Mkataba wa madaktari hao na kuwarudisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Amesema kuwa wamefikia hatua hiyo kwa kuwa madaktari hao wamekiuka , kuvunja mkataba wawalioingia na hospitali hiyo pia kukiuka kanuni za kudumu za Umma na toleo la 2009, kifungu namba F16- F. 17 na F27.
Amesema kuwa madaktari hao waliandikiwa barua ya mara ya kwanza ya kuwaita ili wakutane na Mwenyekiti wa bodi hiyo ya rufaa mbeya lakini walikaidi na kuandikiwa barua ya pili ya kuwataka waeleze kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kutofika kazini kwa siku tano lakini nayo waliikaidi.
Dr. Sigalla akizungumzia kuhusu madaktari 18 ambao ni waajiriwa pia wamo katika mgomo huo alisema kuwa nao wanakabidhiwa barua zao za kusimamishwa ajira zao hospitalini hapo na kuwarudisha Wizarani kwa katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kwa hatua stahiki za kinidhamu.
Hata hivyo imeshuhudiwa baadhi ya madaktari hao wakiondoka kwenye mabweni yao huku madaktari hao wakisikika wakisema wapo tayari kurudi walikotoka na kwamba hawapo kuvumilia kile kinachoendelea hivi sasa.
Wakati huohuo Jeshi la Polisi mkoania hapa lilizingira eneo la Hospitali ya Rufaa kuimarisha ulinzi na usalama.
No comments:
Post a Comment